Ecrit par & déposé en vertu de غير مصنف.

TAMKO NAMBA 27, TAREHE 2/10/1442AH SAWA NA TAREHE 13/5/2021

 

TAMKO LA UMOJA WA WANAVYUONI WA AFRIKA KUHUSU HALI ILIVYO KATIKA MSIKITI MTUKUFU WA AQSA NA PALESTINA KWA JUMLA
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU, MWINGI WA REHEMA, MWENYE KUREHEMU

 

Wa kuhimidiwa ni Allah Mola Mlezi wa viumbe vyote, na rehema na amani zimshukie Mtume wa Mwisho, Muhammad, Familia yake na Swahaba wake wote.

 

Hakika, Msikiti Mtukufu wa Aqsa ni Qibla cha kwanza cha Waislamu na pia ni mahali alipo paishwa Mtume Muhammad (s.a.w.) kwenda mbinguni. Msikiti huu una nafasi kubwa sana katika nyoyo za Waislamu wote ulimwenguni. Kwa muda unaozidi miaka sabini, Msikiti huu uliopo katika Ardhi iliyobarikiwa ya Palestina umekuwa mahali pa majaribu na mitihani kwa umma wa Kiislamu, kwa sababu ya uvamizi wa Wazayuni kwa Palestina na majaribio yao ya mara kwa mara ya kuuvunja na kujenga hekalu lao wanalodai.

 

Mnamo mwishoni mwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na katika siku za Id Elfitri Almubarak ya mwaka huu wa 1442AH, Waislamu walifuatilia kwa masikitiko makubwa uadui uliokuwa unafanywa na Wazayuni kwa Waislamu waliokuwa wanaswali katika Msikiti Mtukufu wa Aqsa kisha vikafuatia vita vikali walivyopigwa Wapalestina waliokuwa wakitetea haki yao na haki ya Waislamu kwa jumla hasa katika ukanda wa Gaza.

 

Umoja wa Wanavyuoni wa Afrika kufuatia ujumbe wake, malengo yake na kuungana kwake na Waislamu wote ulimwenguni, unatoa Tamko hili na kusisitiza yafuatayo:-
1. Tunapinga na kulaani vikali maovu na maonevu ya Wazayuni walowezi wanayoyafanya dhidi ya Wapalestina, ikiwa ni pamoja na kupora ardhi, kuharibu miji na mauaji ambayo hayakuacha hata watoto wadogo.

 

2. Tunakemea nchi na makundi yanayounga mkono utawala wa Kizayuni katika uadui na uovu wake kwa Palestina. Uungaji mkono huu tunauzingatia kwamba ni dalili ya uadui kwa Uislamu na ni kudharu haki za binadamu.

 

3. Tunatoa wito wa kuongeza juhudi katika kuwafahamisha Waislamu nafasi ya Msikiti Mtukufu wa Aqsa na umuhimu wa Palestina kwamba ni masuala yanayowahusu Waislamu wote. Juhudi hizi zifanyike kupitia hotuba za Ijumaa, vipindi vya kuelimisha katika vyombo vya vyombo vya habari na kadhalika.

 

4. Tunawaomba Waislamu wote Afrika na ulimwenguni kuwasaidia Wapalestina katika mapambana yao dhidi ya uadui wa Wazayuni kwa kile mtu anachoweza, hata kama ni kwa kuwaombea katika sala za Ijumaa, sala za Jamaa na katika ibada za faragha.

 

5. Tunawausia na kuwaomba Maimamu wa Msikiti kuleta Kunuti ili kumuomba Allah awaondoshee ndugu zetu masaibu haya makubwa na awape ushindi dhidi ya wavamizi.

 

Mwisho, tunamuomba Allah awanusuru waliosimama kidete katika kuutetea Msikiti Mtukufu wa Aqsa. Hakika, Allah ndiye Mwenye nguvu, Mwenye nguvu kubwa, na rehema na amani zimshukie Mtume wetu Muhammad, Swahaba wake na Familia yake.

 

RAISI WA UMOJA WA WANAVYUONI WA AFRIKA       KATIBU MKUU WA UMOJA WA WANAVYUONI WA AFRIKA
Dr. Seydou Madibaba SYLLA                                                                         Dr. Said Bourhani Abdallah 

 

 

Laisser un commentaire

Votre adresse de messagerie ne sera pas publiée. Les champs obligatoires sont indiqués avec *