Ecrit par & déposé en vertu de غير مصنف.

TAMKO LA UMOJA WA WANAVYUONI WA AFRIKA KUHUSU ZIARA ZA BAADHI YA MAIMAMU NA WALINGANIAJI KUTOKA AFRIKA KWENDA DOLA YA KIZAYUNI INAYOIKALIA KWA MABAVU ARDHI YA PALESTINA

 

Namba ya Tamko: 32       

   
Tarehe: 20/6/1447H sawa na 12/12/2025

 

Himdi zote ni kwa Mwenyezi Mungu Mwenye kusema kuwa: “Na Waumini wanaume na waumini wanawake ni walinzi (washirika wa karibu) wao kwa wao…”. Sura Attawba (9), Aya ya 71. Na rehema na amani zimshukie Mtume wetu Muhammad () Mwenye kusema kuwa: “Waumini katika kupendana kwao na kuhurumiana kwao na kushirikiana kwao kihisia ni kama mwili mmoja …”. Hadithi hii imepokewa na Bukhari na Muslim.
Pia rehema na amani iwashukie Ahlul-Bayt wake (Familia yake), Maswahaba wake na wenye kuwafuata wao kwa wema hadi Siku ya Malipo.

 

Ama baada ya hayo:

Kwa kuzingatia jukumu la kidini lililo juu ya Umoja wa Wanavyuoni wa Afrika, kwa kuzingatia wajibu wake wa kimaadili na kitaaluma, kwa kuhuisha ibada ya nasaha na kuusiana haki, kwa kuutetea Msikiti Mtukufu wa Al-Aqsa na kwa kuunga mkono mapambano ya ndugu zetu wa Palestina dhidi ya ukaliaji wa kidhalimu,
Umoja wa Wanavyuoni wa Afrika unatoa tamko hili kuhusu tukio la ziara za baadhi ya maimamu na viongozi wa dini wa Kiislamu kutoka Afrika kwenda Palestina inayokaliwa kwa mabavu, kupitia safari zilizopangwa na kufadhiliwa na dola ya Kizayuni kwa madai ya kuwaonesha hali halisi huko na kuwafanyia ziara elekezi za kitalii (zilizopangwa kwa lengo maalumu), ikiwa ni kuimarisha udugu na uvumilivu wa kidini, kwa mujibu wa propaganda za Kizayuni.

Kwa msingi huo, Umoja unatangaza kukataa kabisa na kulaani vikali ushiriki wa baadhi ya maimamu na viongozi wa dini wa Kiislamu kutoka nchi kadhaa za Afrika katika ziara hizi zenye shaka, na unaeleza msimamo wake katika mambo yafuatayo:

  1. Kwa hakika kabisa, imethibiti na kubainika kwa Umoja wa Wanavyuoni wa Afrika kuwa, baadhi ya maimamu na viongozi wa dini wa Kiislamu wametembelea dola vaamizi ya Kizayuni, kwa mwaliko wa taasisi za Kizayuni.

  2. Ziara za viongozi na Wanavyuoni waandamizi kwenda katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu katika mazingira haya, katika wakati huu na kwa aina hii ya mwaliko, ni kosa kubwa na anguko hatari linalohitaji ufafanuzi na hata kuomba radhi kwa umma wa Kiislamu, kwa sababu ni uasi wa makubaliano ya Wanavyuoni wa Umma na msimamo wa Waislamu kwa ujumla. Wenye kushiriki katika ziara hizi hawawakilishi msimamo wa Waislamu wa Afrika kuhusu ndugu zao wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

  3. Ni hakika kwamba, ziara hizi zinaashiria kuzipa mamlaka dhalimu za Kizayuni uhalali ambao hazina.

  4. Umoja wa Wanavyuoni unaona kuwa, ziara hizi zinaweza kuwekwa kama aina fulani ya kufanya hali ionekane ya kawaida (normalization), jambo linaloihamasisha dola vamizi (ya Kizayuni) kuendelea na vitendo vyake vya kinyama dhidi ya watu wasiokuwa na hatia na ndugu zetu wa Palestina.

  5. Umoja wa Wanavyuoni unatoa wito wa haki ya kupambana kwa aina zote za mapambano halali ili kuondoa ukaliaji wa mabavu katika Palestina yote kwa ujumla, na katika Msikiti Mtukufu wa Al-Aqsa kwa namna ya pekee.

  6. Umoja wa Wanavyuoni unatoa wito kwa Waislamu wote kuchukua hatua za kuzuia kurejea kwa ziara kama hizi, kwa kutekeleza wajibu wa kutoa nasaha kwa hekima na njia nzuri zaidi.

  7. Umoja wa Wanavyuoni unalaani misimamo ya nchi na taasisi zinazounga mkono Palestina kukaliwa kwa mabavu, kwa kuwa hilo ni kuendeleza dhuluma inayoendelea dhidi ya watu wa Palestina kwa miongo kadhaa, na iliyosababisha migogoro na misukosuko mingi duniani hadi leo.

  8. Umoja wa Wanavyuoni unatangaza nia yake ya kutoa fatwa ya kisheria kutoka Kamati yake ya Fatwa kuhusu hukumu ya kuzuru maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, kwa mwaliko wa mamlaka za wavamizi, pamoja na athari na hukumu zinazofuatia.

  9. Mwisho, Umoja wa Wanavyuoni unawahimiza Waislamu wote kuwaombea wanavyuoni wao dua ya mafanikio, uongofu na kufanya yaliyo sahihi katika kauli, misimamo na maamuzi.

Rehema, amani na baraka zimshukie Mtume wetu Muhammad, pamoja na Ahlul-Bayt wake na Maswahaba wake wote.

Dkt. Said Burhan Abdallah                                         Dkt. Said Baba Sylla

      RAIS                                                                        KATIBU MKUU

 

Laisser un commentaire

Votre adresse de messagerie ne sera pas publiée. Les champs obligatoires sont indiqués avec *